

16 February 2025, 10:32 am
Haya ni mapitio ya utekelezaji wa shughuli za Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) Mkoa wa Mtwara kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2024.
Na Musa Mtepa
Baadhi ya watendaji katika Halmashauri mbalimbali mkoani Mtwara wametakiwa kuhakikisha elimu ya malezi, makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto inafikia jamii na wadau kwa ujumla.
Haya yamejiri wakati wa mkutano wa mapitio ya utekelezaji wa shughuli za Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) Mkoa wa Mtwara kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2024. Mkutano huu umefanyika Februari 14, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Boma, ulio katika ofisi za Mkuu wa Mkoa, na kukutanisha watendaji na wadau mbalimbali.
Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Theresia Ngonyani, amesisitiza umuhimu wa elimu hii kufika kwa kila mdau ili kusaidia kulea watoto kwa namna itakayokuwa bora katika ukuaji wao.
Aidha ameongeza kuwa, kupitia malezi bora, jamii itaweza kuzaa raia wema wenye maadili na kufanya matendo mema.
Katika malengo ya mpango huu, watendaji wamekumbushwa kuhakikisha wanazifikia shule za awali na vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (Baby Cares),pia Watendaji wametakiwa kufikia malengo ya mpango kwa kuwafikia watoto kutoka umri wa miaka 0 hadi 8.
Meneja Uchechemuzi wa Mtandao wa Malezi na Makuzi ya Watoto Nchini (TECDEN), Bruno Ghumpi, amesema kuwa watoto chini ya miaka mitano nchini, asilimia 47 wako katika ukuaji sahihi, huku asilimia 53 hawako katika ukuaji sahihi, hali inayohitaji jitihada kubwa katika sekta hii.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (MTWANGONET) mkoani Mtwara, Fidea Luanda, ameshauri kuwepo kwa utaratibu unaoruhusu kutaja watoto wenye mahitaji maalumu kwa usawa, ili kuhakikisha usawa katika elimu hii.
Mwenyekiti wa Baby Cares Mkoa wa Mtwara, Selemani Mkonga, alisisitiza umuhimu wa kushirikisha vituo vya Baby Cares katika mikutano na wazazi, ili kuboresha utoaji wa elimu hii. Mkoa wa Mtwara unajumla ya Baby Cares 180, na Mkonga ametoa wito wa ushirikiano zaidi katika kuhakikisha kuwa elimu ya malezi inafikia watoto wote.
Sauti ya selemani Mkonga mwenyekiti wa Baby cares mkoa wa Mtwara