Wazazi Wasisitizwa Kupeleka Watoto Shule mkoani Mtwara
15 October 2024, 22:30 pm
Siku ya Mwanamke anayeishi vijijini huadhimishwa October 15, ya kila Mwaka kwa lengo la kutambua mchango wa mwanamke anayeishi vijijini katika jitihada za kujiletea maendeleo yao na kuondokana na umasikini kiwa ni Pamoja na ushiriki wa kuinua Uchumi wa taifa,mtu binafsi na familia
Na Musa Mtepa
Wazazi wametakiwa kuwapeleka watoto wao shule ili kupata elimu itakayowasaidia kukabiliana na fursa mbalimbali zinazojitokea mkoani Mtwara na kuepuka kuwa wasindikizaji wa fursa hizo.
Wito huu umetolewa leo, Oktoba 15, 2024, na mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke aishiye kijijini yaliyofanyika katika Kijiji na kata ya Chawi, halmashauri ya Mji Nanyamba.
Kanali Sawala ammesisitiza kwamba watoto wasiokuwa na elimu wataweza kuwa jamii inayolalamika, kwani fursa zote, iwe binafsi au katika sekta za umma, zinahitaji watu waliopata elimu.
Aidha, ameongeza kuwa serikali inawatambua na kuwajali wanawake wanaoishi vijijini, na juhudi mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kuandaa mikakati ya kuwawezesha kielimu ili kuleta usawa wa kimaendeleo na amani nchini.
Baltazar Komba, mwakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali la Baraza la Taifa (NACONGO), ametoa wito kwa maafisa wanaotoa mikopo kuzingatia vikundi vya wanawake wa vijijini, hasa wale wenye miradi inayokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Baadhi ya wanawake wa Kijiji cha Chawi wameeleza changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa wanaume katika kuwalea watoto na kutoshirikishwa katika matumizi ya fedha zinazopatikana kupitia kilimo cha zao la korosho.