Kamati ya usalama Mtwara yafanya ukaguzi bandarini
7 November 2024, 22:16 pm
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassani alipofanya ziara mwaka jana aliagiza viongozi wa mkoa na taifa kwa ujumla kuhakikisha korosho zote zinazo zalishwa katika mikoa ya Kusini Lindi,Mtwara na Ruvuma zote zinasafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara na utekelezaji wake umeendelea pia katika msimu huu wa 2024/2025
Na Musa Mtepa
Kamati ya usalama ya Mkoa wa Mtwara, chini ya Mwenyekiti wake mkuu wa mkoa, Kanali Patrick Sawala, leo, tarehe 7 Novemba 2024, imefanya ziara ya ukaguzi katika Bandari ya Mtwara ili kujiridhisha na mwenendo wa usafirishaji wa zao la korosho.
Akizungumza baada ya ukaguzi, Kanali Sawala amesema kuwa ziara hiyo ni ya kawaida na kwamba amekuwa akifanya ziara kama hizi mara kwa mara pamoja na kamati ya usalama ili kuona uendelezaji wa shughuli za uhudumiaji shehena, hasa katika msimu huu wa korosho.
Kanali Sawala ametoa wito kwa wanunuzi na wasafirishaji wa korosho kuhakikisha wanatuma mzigo wao mapema kutoka maghalani kuu na kuleta bandarini, akisema kuwa kamati imejiridhisha kuwa bandari iko tayari kuhudumia shehena zote.
Amesisitiza kuwa Bandari ya Mtwara inao uwezo wa kutosha kufanya shughuli zake kwa ufanisi na hakuna sababu ya kusafirisha korosho kwa njia nyingine yoyote zaidi ya kutumia bandari hiyo.
Aidha, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, ameeleza kuwa hadi kufikia leo, Novemba 7, 2024, bandari imeshahudumia meli 11 na kupokea makasha matupu 6,222.
Vilevile, ameongeza kuwa makasha yaliyofungashwa korosho yanafikia 1,000 na shughuli za usafirishaji zinakwenda vizuri, ikizingatiwa kuwa bandari ina uwezo wa kuhudumia zaidi ya tani bilioni mbili kwa mwaka.