Jamii FM

Wakazi kijiji cha Naumbu walia na changamoto ya maji

7 March 2025, 16:21 pm

Mzee Abdala Ulaya akinywa maji kutoka kisima cha asili cha Samwange kilichopo katika kijiji cha Naumbu kusini ikiwa sehemu ya kuwathibitishia waandishi kuwa maji hayo yanatumiwa na Wananchi (Picha na Musa Mtepa)

Kijiji cha Naumbu kipo kata ya Naumbu halmashauri ya Mtwara Vijijini ambacho kwa upande wa mashariki kimepakana na Bahari ya hindi na upande wa Magharibi imepakana na Kijiji cha kitope na kijiografia ya Kijiji hicho kimetawaliwa na miamba mikubwa ya mawe na sehemu chache ya ardhi imejawa na maji yenye asili ya chumvi.

Na Musa Mtepa

Wananchi wa Kijiji cha Naumbu, kilichopo kata ya Naumbu wilaya na mkoani Mtwara, wameiomba Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MTUWASA) kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi wanayokutana nayo katika kijiji hicho.

Wakizungumza na Jamii FM, wananchi hao wamesema kuwa hali ya upatikanaji wa maji imekuwa mbaya kuliko ilivyokuwa hapo awali, kabla ya mradi wa maji kuanzishwa na kuendeshwa na MTUWASA.

Wameeleza kuwa kwa sasa, maji yanapatikana mara mbili au tatu tu kwa mwezi, hali inayowalazimu kutumia maji ya kuokota  kwenye vidimbwi na visima vya asili ambavyo sio salama kiafya.

Kisima cha Asili cha Samwange kinachotegemewa na wananchi wa kijiji cha Naumbu kupata maji ya kunywa na matumizi mengineyo ya nyumbani(Picha na Musa Mtepa)

Halima Bakari na Salumu Mpate, ambao ni wananchi wa Kijiji cha Naumbu Kusini, wamesema kwamba huduma ya maji ilikuwapo kwa uhakika kabla ya MTUWASA kuanza kusimamia mradi huo. Hata hivyo, wameongeza kuwa baada ya kusimamiwa na MTUWASA , hali imekuwa mbaya zaidi na wananchi sasa wanatumia maji ambayo sio salama kiafya kutoka kwenye visima vya asili.

Sauti ya 1 wananchi wa Naumbu kusini

Jamii FM Redio ilifika katika kisima cha asili cha Samwange kinachotumiwa na wananchi wa kijiji hicho kuchota maji ambako ilikutana na Mzee Abdala Ulaya, mkazi wa Kijiji cha Naumbu Kaskazini (Mkungu joma), ambaye ameeleza kuwa kutokana na changamoto ya maji, wananchi wanajikuta wakilazimika kutumia kisima hicho kilichozalisha maji yasiyokuwa salama.

Sauti ya 2 mzee Abdala Ualaya makazi wa Kijiji cha Naumbu kaskazini

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Naumbu Kusini, Selemani Shineni, amesema kwamba tatizo la maji katika kijiji hicho ni kubwa, ingawa halijawahi kujadiliwa kwenye mikutano ya kijiji. Hata hivyo, amesema kuwa yeye kama mwenyekiti amekuwa akifuatilia suala  kwa mamlaka ya maji, lakini majibu anayoyapata hayajakidhi matarajio ya wananchi wa kijiji hicho.

Sauti ya Selemani Shineni Mwenyekiti wa Kijiji cha Naumbu kusini

Akizungumzia hali hiyo kupitia khomein online tv , Iman Semvua, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MTUWASA), ametoa pole kwa wakazi wa Kijiji cha Naumbu na kuwaahidi kuwa changamoto hiyo itapata suluhisho hivi karibuni.

Sauti ya Iman Semvua kaimu mkurugenzi MTUWASA.

 Mradi wa maji wa Kipokoso unaotekelezwa na MTUWASA unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka huu, na kwamba mradi huo utaondoa kabisa changamoto ya maji katika Kijiji cha Naumbu.