Jamii FM
Jamii FM
7 March 2025, 07:57 am

Haya yamejiri kwenye tamasha la michezo lililoandaliwa na shirika la Sports Development Aid likihusisha wanafunzi wa shule za sekondari za Likombe na Chuno zilizopo Manispaa ya Mtwara Mkindani likiwa na lengo la kufikisha ujumbe kupitia michezo wa kuepukana na ukatili na usawa wa kjinsia katika jamii
Na Musa Mtepa
Wanafunzi Mtwara wameaswa kutojihusisha katika mapenzi wakiwa bado masomoni ili kufikia malengo yao ya kielimu.
Akizungumza March 4 , 2025 kwenye tamasha la michezo lililoandaliwa na shirika la Michezo la Sports Development Aid(SDA) kwa kushirikiana na TASA na SSDM, Bi Zainabu Kibunju, kungwi wa mjini Mtwara, amewashauri wanafunzi wa kike na wa kiume kuepuka kujihusisha kimapenzi wakiwa mashuleni, kwani kufanya hivyo kunaweza kuathiri uwezo wao wa kufanya vizuri katika masomo.
Aidha, Bi Kibunju amewataka wanafunzi kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi na walimu wao, hususan walimu wa field, ambao kwa baadhi ya tafiti zisizo rasmi zimeonyesha kuwa wamekuwa wakijihusisha kimapenzi na wanafunzi, jambo linaloleta madhara kama kupata ujauzito na kukatisha masomo.

Paulina Lidasi, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu kutoka Shule ya Sekondari Likombe, amekiri changamoto za walimu na bodaboda kuwa na mahusiano kimapenzi na wanafunzi na kuahidi kukabiliana na changamoto hizo kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushirikisha viongozi wa kiserikali.
Maila Bashiru, mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Chuno, amesema kwamba wasichana wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi kutoka kwa wanaume, ikiwa ni pamoja na kupewa fedha na chips ikiwa njia ya kuwashawishi kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na kueleza kuwa kupitia mafunzo ya Bi Kibunju, wataweza kujiepusha na changamoto hizo.
Kwa upande mwingine, Ali Mvita, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Likombe, amezungumzia kuhusu umuhimu wa kujua malengo yake na jinsi ya kuyafikia huku akisisitiza umuhimu wa jamii na serikali kulinda watoto wa kiume dhidi ya vitendo vya ubakaji.
