Jamii FM
Jamii FM
7 January 2026, 19:27 pm

Wananchi wa Makome B wameiomba Serikali kupitia RUWASA kukamilisha mradi wa maji uliosimama ili kumaliza uhaba wa maji safi unaosababisha magonjwa na changamoto za kijamii.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa kijiji cha Makome B kilichopo kata ya Mbawala,Halmashauri ya Mtwara vijijini, Mkoani Mtwara wameiomba Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilisha mradi wa maji unaojengwa katika kijiji hicho ili kuondokana na adha ya uhaba wa maji safi na salama inayowakabili.
Wakizungumza na waandishi wa habari January 6 ,2026 wananchi hao wamesema kuwa kutokana na kukosekana kwa maji safi na salama, wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali za kiafya na kijamii, hali inayotokana na matumizi ya vyanzo vya maji vya asili ambavyo si salama kwa matumizi ya binadamu.
Wakazi wa kijiji hicho, Mwanahamisi Mitole na Sinani Kibwana, wamesema tatizo la maji limesababisha kuongezeka kwa magonjwa ya tumbo, hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali pamoja na migogoro ya kifamilia, hali inayohatarisha ndoa zao. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wameomba wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilisha mradi wa maji uliosimama katika kijiji hicho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Makome B, Ndugu Salumu Liwingu, amekiri kuwa hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hicho ni mbaya, kwani wananchi wanategemea maji yanayotiririka kutoka maeneo mbalimbali ambayo si salama, hali inayochangia wananchi kupata magonjwa ya tumbo mara kwa mara.

Akizungumzia mradi wa maji unaojengwa kijijini hapo, Mwenyekiti huyo amesema mradi huo umeingia mwaka wa tatu tangu kuanza kwake. Ameeleza kuwa mradi huo ulizinduliwa rasmi mwaka 2024 wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, lakini maji yalitoka kwa takribani dakika tano pekee na tangu hapo hakuna maji yaliyowahi kutoka tena.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mtwara, Abdulaziz Hemedi, amesema mradi wa maji wa Makome umefikia asilimia 65 ya utekelezaji, huku asilimia 41 ya fedha za mradi zikiwa tayari zimeshalipwa kwa mkandarasi. Amesema changamoto mbalimbali zimejitokeza na kusababisha mradi huo kushindwa kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa Makome A na B, hali iliyopelekea RUWASA kufikiria kuvunja mkataba na mkandarasi husika.

Aidha, amesema mkataba wa ujenzi na ukamilishaji wa mradi huo ulitarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2025, na kufikia wakati wanapofikiria kuvunja mkataba, utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 65.

Hata hivyo, Kaimu Meneja huyo amesema pamoja na mchakato wa kuvunja mkataba na kumpata mkandarasi mpya wa kukamilisha mradi huo, wananchi wa vijiji vya Makome A na B wanatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Maji na ofisi mbalimbali za Serikali, hadi kufikia mwezi Julai 2025 upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya vijijini umefikia asilimia 83 na Sera ya Taifa ya Maji ikisisitiza upatikanaji endelevu wa maji safi na salama kwa kuhusisha jamii, sekta binafsi pamoja na kulinda rasilimali za maji ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wote wa vijijini.
