Jamii FM
Jamii FM
5 March 2025, 07:20 am

Kata za Msimbati na Madimba ni kata ambazo nishati ya gesi asilia inapozalishwa na kuchakatwa hivyo ujenzi wa kituo cha afya ni sehemu ya utekelezaji wa CSR kwa wananchi kutoka na shughuli za uzalisha ji wa gesi asilia.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Kata ya Msimbati wameshukuru na kuipongeza serikali kwa ujenzi na ufunguzi wa Kituo cha Afya Msimbati, kwani hapo awali walikumbana na changamoto kubwa ya kutembea umbali mrefu ili kupata huduma za afya.
Issa Mfaume Chande, Mzee wa Kijiji cha Msimbati, amesema kabla ya ujenzi wa kituo hicho, walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya. Hivyo, ufunguzi wa kituo hicho utawasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto hiyo.
Fatuma Waziri na Zaituni Lipemba, kwa upande wao, wameelezea furaha yao kwa kupata huduma za afya karibu, kwani hapo awali walikuwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu na kwa gharama kubwa ili kufuata huduma hizo. Wamesisitiza kuwa ujenzi wa kituo hicho umeleta nafuu kubwa kwao.
Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Msimbati, Henri Hatia, ameelezea kuwa uwepo wa kituo hicho umepunguza kwa kiasi kikubwa umbali kwa wananchi wa vijiji vya Msimbati, ambao sasa wanapata huduma za afya kwa urahisi zaidi.
Dkt. Henri ameongeza kuwa tangu kufunguliwa kwa kituo hicho na kuanza kutoa huduma rasmi, kila siku zaidi ya wananchi 17 hadi 20 wanapata huduma za afya katika kituo hicho.
Kituo cha Afya Msimbati ni matokeo ya ziara ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, alipotembelea Kata ya Msimbati na Madimba ili kujionea changamoto mbalimbali kwa Wananchi ambapo aligundua kuwepo kwa changamoto ya kutokuwepo kwa kituo cha afya, ukosefu wa taa za barabarani, na uhaba wa umeme wa uhakika.
Dkt. Biteko alitoa maagizo ya kuanza mchakato wa kutekeleza miradi ya kuboresha huduma za afya na miundombinu katika maeneo hayo.