Mudy Ray: Aahidi Mifuko ya Saruji na Vifaa vya Michezo,Shule ya Msingi Ruvula
3 November 2024, 10:57 am
Hapo awali shule ya msingi Ruvula ilikuwa shule shikizi ambapo mwaka 2023 ilipata usajili rasmi wa kutambulika kuwa shule kamili na mwaka 2024 kwa mara ya kwanza imehitimisha wanafunzi 20 wa darasa la saba huku 17 kati yao wakielekea kidato cha kwanza.
Na Musa Mtepa
Wanafunzi 20 wa darasa la saba wa shule ya msingi Ruvula, iliyoko kata ya Msimbati, halmashauri ya Mtwara Vijijini, wamefanya maafali yao ya kwanza tangu shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 2018.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Zainabu Selemani, mwanafunzi na muhitimu wa shule hiyo, ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake, shule imefanikiwa kufaulisha wanafunzi 17 kati ya 20 waliohitimu elimu ya msingi mwaka 2024.
Zainabu pia ametaja changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi, ikiwemo uhaba wa vifaa vya michezo, ukosefu wa nyumba za walimu, na nyumba ambayo haina sakafu iliyosakafiwa pamoja na ukosefu wa umeme.
Kwa upande wake, Musa Mpiko, akimwakilisha mgeni rasmi, Bw. Mohamedi Abdala Mohamedi (Mudy Ray), ambaye ni mdau wa maendeleo na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mtwara, ameahidi kutoa mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa sakafu ya nyumba ya mwalimu, vifaa vya michezo, pamoja na fedha shilingi laki mbili na kwa ajili ya fundi.
Pia, Musa Mpiko ameahidi kugharamia mahitaji ya kuanzia kidato cha kwanza kwa watoto wa kike watakaofanikiwa kuwa katika kumi bora ngazi ya mkoa katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kutoka shule ya msingi Ruvula.