Bashe azindua kiwanda cha kubangua korosho Mtwara
2 October 2024, 23:45 pm
Takribani Bilioni 3.4 inaelezwa kuwa zimetumika kujenga kiwanda hicho huku ikikadiriwa kuwa na uwezo wa kubangua korosho tani 3,500 kwa mwaka
Waziri wa Kilimo, Mh. Hussein Bashe, amezindua rasmi kiwanda cha kubangua korosho cha Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba, Newala (TANECU LTD), kilichojengwa katika Kijiji cha Mmovo, wilaya ya Newala mkoani Mtwara.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Bashe avitaka vyama vya ushirika kubadilika ili viweze kujiendesha bila kutegemea ushuru kutoka kwa wakulima pamoja na bodi inayosimamia kiwanda kuto ingiliwa na kuwa huru ku iweze kufanya biashara kwa ufanisi.
Waziri Bashe amewahakikishia wakulima kwamba serikali itasimamia bei ya korosho kwa msimu wa 2023/2024, kuhakikisha inalingana na mwenendo wa soko la dunia.
Mbunge wa Tandahimba, Ahamad Katani, amemuomba Waziri Bashe kuzingatia gharama zinazowakabili wakulima wa korosho, akihitaji serikali kutafuta bilioni 68 ili kusaidia TANECU kutatua changamoto hizo.
Kujengwa kwa kiwanda hiki ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya TANECU ya kujenga viwanda 20, ambapo 10 vitajengwa wilaya ya Newala na 10 vingine wilaya ya Tandahimba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza thamani ya zao la korosho.