Jamii FM

Vijana 69 mkoani Mtwara wahitimu  mafunzo ya ufundi stadi

2 March 2025, 11:23 am

Bi Theresia Mosha akimkabidhi cheti muhitimu wa mafunzo ya ufundi stadi katika maafali ya kutamatisha mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza (Picha na Msafiri Kipila)

Hizi ni sherehe za kuhitimu  kwa mafunzo ya ufundi stadi ambapo takribani vijana 69 wamehitimu na kutunukiwa vyeti ikiwa ishara ya kutambuliwa kwa mafunzo hayo,mafunzo haya yalikuwa yanatolewa kwa mafundi chuma,seremala na mafundi uchoraji

Na Msafiri Kipila

Vijana 69 kutoka mkoani Mtwara, wakiwemo wanaume 54 na wanawake 15, wamemaliza mafunzo yao katika fani mbalimbali za ufundi stadi, ikiwa ni pamoja na ucharaji, uchongaji, fundi chuma, na fundi seremala.

Mafunzo haya, ambayo yamefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) pamoja na Shirika la Alwaleed, yalianza kutolewa tangu mwezi Novemba mwaka 2024 yakilenga kuimarisha Sanaa na Utamaduni kwa vijana kupitia ufundi stadi pamoja na kutoa fursa za ajira kwa vijana.

Mkurugenzi wa Shirika la ADEA, Saidi Chilumba, amesema kuwa mafunzo hayo yana faida kubwa kwa vijana kwani kupitia ubunifu wa hali ya juu walioupata, wataweza kutengeneza bidhaa mbalimbali na kujipatia kipato cha kujitegemea.

Sauti ya Saidi Chilumba Mkurugenzi wa ADEA

Nao baadhi ya wahitimu wameelekeza shukrani zao kwa mashirika ya UNESCO, Alwaleed na ADEA kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewapa fursa kubwa katika maisha yao kwa waongezea ujuzi ambao wataenda kuutumia katika kazi zao kwa ustadi mkubwa.

Sauti ya baadhi ya wahitimu wa mafunzo

Theresia Ibrahim Mosha, Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara, kwa niaba ya Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini-Mashariki, ameyashukuru mashirika yote kwa kutoa mafunzo  kwa vijana mkoani Mtwara.

Aidha ameipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu, jambo ambalo limeliwezesha mashirika kutoa mafunzo hayo bila vikwazo.

Sauti ya Theresia Ibrahim mkuu wa VETA Mtwara

Bi Theresia Ibrahim Mosha amesisitiza kwamba mafunzo hayo ni muhimu  kwa vijana, hususani kwa mkoa wa Mtwara ambapo kipindi cha nyuma, mafunzo kama hayo hayakuwa yanapatikana kwa urahisi.