Nuru FM

DC MOYO akiri Kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa vyumba vya Madarasa Mlolo na Kiponzelo

1 December 2022, 7:11 am

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akikagua moja ya vyumba vya madarasa ambavyo havijakamilika na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake

MKUU wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amesema kuwa hajaridhishwa na ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari katika Tarafa ya Mlolo na Kiponzero na kutoa Siku saba kuhakikisha vyumba vya madarasa hayo viwe vimekamilika.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa, Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Moyo alisema kuwa vyumba vyote vya madarasa vinatakiwa kuwa vimekamilika kabla ya tarehe kumi na tano mwezi wa kumi na mbili kwa ajili ya kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Moyo alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kwenye sekondari zote kwa lengo la kuwapunguzia adha wananchi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa hivyo viongozi walipewa dhamana ya kusimamia wanapaswa kusimamia ujenzi huo kwa wakati.

Alisema kuwa shule zote zilipewa pesa kwa wakati mmoja haiwezekani shule nyingine ndio wanaanza shule nyingine wafikia eneo la kupaua na wengine wanapaka rangi hivyo watakao chelewesha watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Moyo aliwataka viongozi wa shule ambazo wamekabidhiwa majengo vya madarasa yaliyokamilika kuyatunza na kuyakarabati pale inabidi ili kuyafanya madawati hayo yaweze kudumu kwa muda mrefu.

Katika ziara hiyo mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alifanikiwa kutembelea jumla ya shule nane ambazo ni shule ya sekondari Lyasa,Lumuli,Lyandembela,Mgama,Lupembelwasenga,Tanangozi,Isimila na Muhwana