Mpanda FM
Mpanda FM
1 April 2026, 9:49 am

“Lazima tujirekebishe tufanye kazi kwa huruma na upendo”
Na Betord Chove
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ameonesha kutoridhishwa na hali ya uzembe kwa baadhi ya watumishi katika vituo vya afya wilayani humo akiwataka kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua huduma za afya na kutembelea vituo vya afya vya Karema, Kasekese pamoja na zahanati ya Ikola, Buswelu amesema kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi kuhusu utoaji wa huduma hali inayohitaji hatua za haraka kurekebishwa.
Amesisitiza kuwa uzembe wa watumishi haupaswi kuwa sababu ya kuwaumiza wananchi akionya kuwa vitendo hivyo vinaharibu taswira ya serikali kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Buswelu amesema serikali haitavumilia kuona vifo vinavyoweza kuzuilika hususani vya wajawazito akitaka watumishi kuwajibika kikamilifu ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote wa wilaya ya Tanganyika.