Mpanda FM

Skimu ya umwagiliaji Mwamkulu, kicheko kwa wakulima

20 February 2026, 6:16 pm

Picha inayoonesha sehemu ya mradi huo. Picha na Ben Gadau

“walikuwa wakikumbana na changamoto katika shughuli za kilimo, ikiwemo ukosefu wa maji ya uhakika kwa ajili ya umwagiliaji”

Na Ben Gadau – Katavi

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwamkulu wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi wa skimu ya umwagiliaji, wakisema kuwa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha kipato cha wakulima na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha katika eneo hilo.

Wakizungumza katika ziara ya kutembelea miradi iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph, wananchi hao wamesema kuwa hapo awali walikuwa wakikumbana na changamoto katika shughuli za kilimo, ikiwemo ukosefu wa maji ya uhakika kwa ajili ya umwagiliaji, hali iliyokuwa ikiwakwamisha kiuchumi na kuwarudisha nyuma kimaendeleo, hivyo kupitia utekelezaji wa miradi hiyo wana matumaini ya kuinua uzalishaji na kuboresha maisha yao.

Sauti za wananchi wakipongeza kuletwa kwa mradi huo

Awali akisoma taarifa ya mradi huo Eng Saimon Bai Meneja wa Mradi-Mwamkulu mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishai wa mazao ya kilimo kutoka wastani wa gunia 20 kwa ekari hadi gunia 40 kwa ekari pindi utakapokamilika.

Sauti ya msoma taarifa ya mradi huo ambaye pia ni meneja wa mradi Eng Saimon Bai

Mradi wa scheme ya umwagiliaji umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 33.9, ambapo mradi huo utaongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 1,000 hadi hekta 3,000 na ongezeko la wanufaika kutoka wakulima 300 hadi 1,500, sambamba na kuboresha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.

Viongozi mbalimbali akiwemo mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph wakitembelea mradi huo.picha na Ben Gadau