Mpanda FM
Mpanda FM
28 January 2026, 11:05 am

Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph akipanda mti. Picha na Anna Mhina
“Miti hii tuliyoipanda muitunze”
Na Anna Mhina
Wakati Taifa likiadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph amewataka wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti na kutumia nishati safi ya kupikia.
Jamila ametoa wito huo January 27, 2026 alipokuwa mgeni rasmi kwenye zoezi la upandaji miti uliofanyika kando mwa barabara kuu iendayo Tabora kata ya Ilembo manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ikiwa ni maelekezo ya Taifa kwa siku hii ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Dr. Samia.
Awali akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi afisa mazingira msaidizi wa manispaa ya Mpanda Zaituni Rashidi amesema halmashauri imekuwa ikitoa hamasa juu ya umuhimu wa upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi waliohudhuria zoezi hilo akiwemo Happiness Nkondo na Stanslaus Joseph kutoka shule ya sekondari Nsemulwa wameeleza umuhimu wa kupanda miti ikiwa ni pamoja na kuleta hewa nzuri.
Hata hivyo katika kuazimisha January 27 ya kijani halmashauri ya Mpanda imeandaa jumla ya miche 300 ya mapambo ambapo mpaka kufikia siku hii ya leo jumla ya miti laki sita na arobaini na tano imepandwa katika maeneo mbalimbali.