Mpanda FM
Mpanda FM
17 January 2026, 12:25 pm

Baadhi ya madiwani wakitembelea mradi wa miji 28. Picha na Betord Chove
“Mpango tulioupokea ni mzuri shida ya maji katika mji wetu tunakwenda kuipunguza”
Na Betord Chove
Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mpanda imetoa taarifa ya utendaji kazi kwa baraza la madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Mpanda ili waweze kutambua hali ya upatikanaji wa maji na miradi inayotekelezwa.
Wakizungumza mara baada ya kikao kazi hicho kilichohusisha kutembelea mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa kata ya Shanwe baadhi ya madiwani wamesema kuwa hatua hiyo imeongeza uwazi na itasaidia kuwafanya wananchi kufahamu hatua zinazoendelea katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Rehema Nelson mkurugenzi mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mpanda ameainisha lengo la kukutana na madiwani wa manispaa ya Mpanda ni kushirikiana nao ili waweze kuainisha changamoto zilizopo katika kata zao ili waziingize kwenye bajeti.
Akizungumzia kuhusiana na hali ya upatikanaji wa maji mstahiki meya wa manispaa ya Mpanda Charles Venancy Filipo amesema ofisi yake itaongeza msukumo wa upatikanaji wa pesa za malipo kwa mkandarasi ili akamilishe mradi wa miji 28 kwa wakati ili wananchi wa manispaa ya Mpanda wapate maji kwa uhakika.
Kwa sasa maji yanayozalishwa ni lita milioni 6 na laki 2 na Mji Wa Mpanda unaupungufu wa maji lita milioni 9.8 ambapo mradi wa maji wa miji 28 utazalisha lita million 12 ambapo matarajio baada ya mradi huu ni kupata jumla ya lita million 18 na laki 2 .