Mpanda FM
Mpanda FM
12 January 2026, 12:27 pm

“Rai yangu kwenu hii miche mkaipande na muitunze”
Na Samwel Mbugi
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph amewahimiza wakulima wa zao la korosho kuhakikisha wanapanda na kuitunza ipasavyo miche waliyoipokea ili iweze kusitawi vizuri na kuleta tija katika maendeleo ya kilimo na kuinua uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Jamila ametoa wito huo wakati wa hafla ya ugawaji wa miche ya korosho kwa wakulima wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi bure hafla iliyoandaliwa ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuwasaidia wananchi wa ngazi zote kuboresha uzalishaji wa mazao ya biashara.
Aidha amewahimiza maafisa ugani katika ngazi ya halmashauri na ngazi za chini kuhakikisha wanawatembelea wakulima mara kwa mara ili kuwapatia elimu ya kina kuhusu utunzaji wa zao la korosho pamoja na kupokea na kutatua changamoto zinazowakabili.
kwa upande wa wakulima wa zao la korosho wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia mbegu bure wakisema kuwa hatua hiyo itachochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima wa manispaa ya Mpanda.
Kwa upande wake kaimu afisa kilimo wa manispaa ya Mpanda Abdallah Towazi amesema kuwa lengo kuu la kuotesha na kugawa miche ya korosho ni kuwainua wananchi kiuchumi na kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia uzalishaji endelevu wa zao hilo.