Mpanda FM
Mpanda FM
7 January 2026, 10:50 am

Mama wa mtoto akiwa amempakata mwanae. Picha na Anna Milanzi
“Tumekuja kumuona huyu mtoto baada ya kupata taarifa”
Na Anna Milanzi
Mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi tisa katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi anakabiliwa na changamoto kubwa ya kiafya baada ya kuugua ugonjwa unaosababisha uvimbe mkubwa mgongoni.
Kwa mujibu wa mama wa mtoto huyo uvimbe huo ulianza kama kipele kidogo lakini kadri siku zilivyoendelea uliendelea kukua na kusababisha maumivu makali hali iliyomfanya mtoto kushindwa kucheza na kulala vizuri kama watoto wengine wa rika lake.
Baada ya kuhangaika kutafuta matibabu katika vituo mbalimbali vya afya bila mafanikio mtoto huyo alifikishwa hospitali ya Rungwa ambapo madaktari walitoa rufaa ya kumpeleka hospitali ya Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya matibabu ya kibingwa. Hata hivyo, rufaa hiyo ilishindikana kutekelezwa mara moja kutokana na mama wa mtoto kukosa fedha za usafiri na gharama za matibabu.
Mpanda Radio FM baada ya kumuona mtoto huyo iliwasiliana na Glady Welfare Organization kutoka jijini Dar es Salaam ambapo mkurugenzi wa taasisi hiyo Gladness Liamuya alieleza utayari wa kusaidia matibabu ya mtoto huyo.
Mama wa mtoto huyo ameishukuru Mpanda Radio FM pamoja na taasisi hiyo ya Glady welfare Organization na watu wote waliojitokeza kusaidia, akieleza kuwa msaada huo umeirejeshea familia yake matumaini mapya.
Mjumbe wa eneo analoishi mama wa mtoto huyo ameishukuru Mpanda radio FM kwa jitihada hizo akisema hatua iliyochukuliwa na redio hiyo imeonesha mshikamano wa jamii katika kusaidia wenye uhitaji.