Mpanda FM
Mpanda FM
20 December 2025, 5:05 pm

“Lakini cha ajabu lile eneo kaingia mtu kalikodisha”
Na John Benjamin
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Milala halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamehoji uhalali wa kuuzwa kwa eneo la makaburi ya kijiji hicho baada ya kubaini kuwepo kwa shughuli za kibinadamu zinazoendelea kufanyika.
Wananchi hao wameibua hoja hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo ambapo wameeleza kuwa kushangazwa na hatua ya serikali ya kijiji kushindwa kuchukua hatua za haraka kuzuia shughuli hizo hali ambayo wamedai inakiuka maadili,mila na maslahi mapana ya kijiji chao.
Akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa kijiji cha Milala Veronika Lemi amesema mgogoro wa eneo la makaburi umekuwa wa muda mrefu na umeendelea kuwa sugu kutokana na changamoto mbali mbali ikiwemo madai ya kuhusika kwa baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji katika mgogoro huo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Misunkumilo Musa Ngogolwa amemwagiza mwenyekiti wa kijiji hicho kumwandikia barua ya zuio wahusika wote wanaodaiwa kuvamia eneo la makaburi huku akisisitiza kuwa shughuli zozote zinazofanyika katika eneo hilo zisitishwa kwani eneo hilo ni mali ya kijiji hicho hivyo halipaswi kutumika kwa shughuli nyingine zozote bila kufuta utaratibu za kisheria na ridhaa ya wananchi.
Aidha Ngogolwa amesema kuwa uongozi wa kata kwa kushirikiana na manispaa ya Mpanda utaendelea kushughulikia mgogoro huo hadi ufumbuzi wa kudumu utakapopatikana huku akisisitiza kuwa hakuna mtu au tasisi itakayoruhusiwa kufanya shughuli zozote kwenye eneo hilo la makaburi kinyume cha sheria.