Mpanda FM
Mpanda FM
15 December 2025, 5:58 pm

“Tukae kwa pamoja tuweke mikakati namna gani ya kupambana na udumavu”
Na Samwel Mbugi
Mkuu wa wilaya ya Mpanda mkoani Katavi Jamila Yusuph amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kusimamia kikamilifu mikakati ya kuhakikisha elimu ya lishe inatolewa kwa wananchi ili kuondokana na tatizo la udumavu kwa watoto wilayani Mpanda.
Jamila ameyasema hayo wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya ya Mpanda (DCC), kilichowakutanisha viongozi kutoka halmashauri ya manispaa ya Mpanda pamoja na halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ambapo amebainisha kuwa kwa sasa Wilaya ya Mpanda ina kiwango cha udumavu cha asilimia 32.
Akitoa taarifa ya lishe kwa upande wa manispaa ya Mpanda afisa mipango Leonard Kilamhama amesema kuwa kwa kipindi cha Julai hadi Novemba jumla ya watoto 52,242 wamepimwa hali ya lishe katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na ngazi ya jamii.
Kwa upande wake Afisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Nsimbo Alfred John amesema kuwa halmashauri hiyo imeandaa mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la udumavu ikiwemo utekelezaji wa afua za lishe na kuhamasisha upandaji wa miti ya matunda kwa wananchi.