Mpanda FM

RC Mrindoko atoa wiki mbili kwa mkandarasi wa daraja la Mirumba

22 November 2025, 11:18 am

Katikati ni mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akikagua ujenzi wa daraja. Picha na Benny Gadau

“Nataka hizo wiki mbili nione kazi ya maana imefanyika”

Na Benny Gadau

Mkuu wa mkoa wa Katavi  Mwanamvua Mrindoko amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa daraja la Mirumba lenye thamani ya zaidi ya billion 6 katika halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.

Akizungumza katika eneo hilo Mrindoko amesema kuwa daraja hilo ni muhimu kwa wananchi kwani litarahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima kwenda mkoa jirani wa Rukwa huku akimpa mkandarasi wiki mbili kuonyesha maendeleo kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utendaji kazi na akisisitiza kuwa hatua kali za kimkataba zitatumika endapo ndani ya muda huo hakutakuwa na mabadiliko yoyote.

Sauti ya mkuu wa mkoa

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Mwakabende amesema mradi unahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 60 katika barabara ya Katete – Kibaoni ambalo ametaja kuwa litaimarisha usafiri wa watu na mizigo, tofauti na daraja lililokuwepo lililokuwa na uwezo mdogo wa kuhimili magari makubwa hasa mvua.

Sauti ya meneja TANROADS

Mkataba wa mradi ni wa miezi 12, kuanzia 27 Novemba 2024 hadi 27 Novemba 2025, na hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 38, ikilinganishwa na muda uliotumika asilimia 91.6, jambo linaloonyesha kuwa kasi ya ujenzi bado ni ndogo, Mradi unafadhiliwa na International Development Association (IDA) kwa gharama ya shilingi bilioni 6.39 (bila VAT), ukitekelezwa na M/s Safari General Business Co. Ltd kwa ushirikiano na Mbuya’s Co. Ltd, chini ya usimamizi wa TANROADS – TECU.