Mpanda FM
Mpanda FM
19 November 2025, 12:01 pm

Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph akikabidhi mbegu kwa mkulima. Picha na Restuta Nyondo
“Sisi kama wilaya tumejipanga kuwawezesha vijana waweze kujiajiri katika kilimo”
Na Restuta Nyondo
Vijana wilayani Mpanda wametakiwa kutumia fursa ya maonesho ya ufunguzi wa msimu wa kilimo mkoa wa Katavi kujifunza mbinu mbalimbali ili waweze kujiajiri kupitia ujuzi katika sekta ya kilimo na mifugo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph wakati alipotembelea maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya ukumbi wa manispaa ya Mpanda na kusema kuwa wilaya hiyo imejipanga kuwasaidia vijana kuwawezesha kujiajiri.
Kwa upande wake Nehemia James katibu tawala msaidizi anayeshughulikia masuala ya uchumi na uzalishaji amesema kuwa wakulima wajitokeze katika maonesho ili kujifunza namna ya kupima udongo na kujiandikisha na kuhakiki taarifa kwaajili ya kupata pembejeo za ruzuku.
Katika hatua nyingine Nehemia amewataka wauzaji wa mbegu na mbolea kutopandisha bei na wanaendelea na ukaguzi ili kubaini vitendo hivyo.
Mkoa wa Katavi kwa mwaka 2025/2026 unatarajia kulima jumla ya hekta 396,448 na kufanya uzalishaji wa tani zaidi ya milioni moja kwa mazao ya chakula na biashara.