Mpanda FM
Mpanda FM
23 June 2025, 12:09 pm

Mto Misunkumilo wananchi wakiendelea na shughuli zao. Picha na Anna Mhina
“Maeneo ya mtoni sio maeneo rafiki kwa watoto”
Na Roda Elias
Mtoto Aliefahamika kwa jina la Barnaba Daniel (7) mkazi wa kata ya Makanyagio manispaa ya Mpanda mkoani Katavi amefariki dunia baada ya kuzama mto Misunkumilo.
Tukio hilo limetokea juni 18 /2025 majira ya saa 6 mchana katika mto misunkumilo eneo la Machinjioni huku chanzo kikidaiwa kuwa mtoto huyo alienda mtoni kwa lengo la kuogelea.
Wakizungumza na Mpanda Radio FM baadhi ya wananchi waliokuwa karibu na tukio hilo wamesema kuwa mtoto huyo ni mgeni katika eneo hilo.
Kwa upande wake mjumbe wa mtaa huo Maneno Joseph ameeleza namna ambavyo alipokea taarifa ya tukio hilo ambapo amesema kuwa alipofika eneo la tukio palikuwa na watu wengi huku nguo za mtoto zikiwa chini.
Naye mwenyekiti wa mtaa huo Ibrahim Mzanda amesema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo alifika eneo la tukio na kukuta wasamalia wema wameutoa mwili wa mtoto mtoni huku akitoa rai kwa wazazi kuwalinda watoto.
Jitihada za kumtafuta kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Katavi David Mutasya zilifanikiwa na kusema kuwa taarifa hizo bado hazijamfikia ofisini kwake.