

24 February 2025, 5:39 pm
Picha ya soko la Machinjioni. Picha na Edda Enock
“Tunashindwa wapi pa kupeleka haja zetu soko halina choo”
Na Edda Enock
Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la machinjioni manispaa ya Mpanda mkoani katavi wametoa malalamiko yao kwa serikali kuhusu hali ya miundombinu mibovu katika soko hilo, licha ya kutoa ushuru kila siku.
Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na Mpanda radio FM ambapo wamesema kuwa hali ya ubovu wa miundombinu, ikiwemo mfumo wa usafi, choo na maji inachangia katika kushindwa kufanya biashara zao na kuathiri huduma wanazotoa kwa wateja
Hamis Msigalo ambae ni diwani wa kata ya Mpanda Hotel akizungumza kwa njia ya simu amesema changamoto inayosababisha kuchelewa kuweka miundombinu ya soko ni pamoja na mdhabuni aliyekuwepo awali kuondoka, hivyo tayari serikali imeshampata mdhabuni kwa ajili ya ukarabati wa soko hilo.
Hata hivyo katika kikao cha mapendekezo ya rasimu ya mpango na bajeti ya halimashauri ya manispaa ya Mpanda kwa mwaka wa fedha 2025-2026 soko la hilo liliwekwa kwenye bajeti ya ukarabati.