

13 February 2025, 11:09 am
“kiongozi huyo ambaye alikuwa mwalimu wa maadili mema, mshauri wa jamii, na kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo.“
Na Anna Mhina -Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, Ameshiriki katika mazishi ya Askofu wa kanisa la New Harvest Church, Dkt. Laban Ndimubenya, February 09 katika kanisa la New Harvest Church, Mikocheni, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Katika hotuba yake, Mrindoko ameeleza kuwa kifo cha Askofu Dkt. Laban ni pigo kubwa kwa Taifa, kutokana na umuhimu wa kiongozi huyo ambaye alikuwa mwalimu wa maadili mema, mshauri wa jamii, na kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo.
RC Mrindoko ameongeza kuwa Serikali itaendelea kumuenzi Askofu Dkt. Laban kwa kuthamini mchango wake na kuendeleza juhudi alizozianzisha katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi, amemuelezea marehemu kama mtu aliyekuwa na maono kwa jamii na mwenye bidii isiyo na kifani katika kupigania maendeleo ya watu wake.
Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Serikali, maaskofu kutoka madhehebu mbalimbali ndani na nje ya nchi, pamoja na wananchi mbalimbali wa mkoa wa Katavi.