RC Katavi apiga stop wakuu wa wilaya kufyeka mazao ya wakulima
6 January 2025, 7:18 pm
“Ameutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kulipa fidia ya mbegu kama sehemu ya uharibifu”
Na Samwel Mbugi -Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko ametoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya kuhakikisha doria zinazofanyika katika misitu na mapori tengefu zisihusishe ufyekaji wa mazao ya wananchi.
Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa ambapo ametumia nafasi hiyo kuutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kulipa fidia ya mbegu kama sehemu ya uharibifu.
Baadhi wa wananchi wa kijiji cha Kagunga kata ya Kasekese halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambao ni wahanga wa kufyekewa mahindi kinyume na makubaliano na serikali ya kijiji wametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa baada ya kutoa kauli ya kupewa fidia ya mbegu.
Ikumbukwe kuwa baada ya tukio la ufyekaji wa mahindi Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu alisema mahindi yaliyofyekwa katika doria hizo ni mahindi na bangi ambazo zinalimwa na wavamizi wa msitu.