Mahindi yafyekwa tena Katavi
26 December 2024, 5:41 pm
“Katika makubaliano ilikuwa wataendelea kufanya shughuli zao za kilimo mpaka watakapopewa fidia lakini hawataruhusiwa kukata mti wowote ambao utakuwa ndani ya shamba“
Na Samwel Mbugi-Katavi
Baadhi wa wananchi wa kata ya Kasekese kijiji cha Kagunga halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wanaofanya shughuli za kilimo katika eneo la mradi wa hewa ukaa wamelalamikia hatua ya kufyekewa mahindi na walinzi wa msitu ikiwa ni kinyume na makubaliano.
Wakizungumza na Mpanda Radio FM wamesema makubaliano yalikuwa walipwe fidia ili kupisha mradi katika maeneo hayo ambapo wameongeza kuwa katika makubaliano ilikuwa wataendelea kufanya shughuli zao za kilimo mpaka watakapopewa fidia lakini hawataruhusiwa kukata mti wowote ndani ya shamba.
Hata hivyo wameongeza kuwa katika makubaliano hayo wao walikubali kuendelea kufanya kazi za kilimo katika maeneo hayo kwa kuzingatia makubaliano ya bila kukata miti na kutokujenga nyumba za kudumu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kagunga Michael John Msenges amebainisha kuwa ni kweli mgogoro huo upo lakini una historia ndefu ya makubaliano na wakulima wa maeneo hayo ambayo yapo kwenye mradi.
Paulos Kija Diwani wa kata ya Kasekese amesema kuwa mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu tangu Mkuu wa Wilaya akiwa Salehe Mhando hivyo wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki wakati suala hilo likiendelea kushughulikiwa ili kila mmoja apate haki yake.
Kija amebainisha kuwa ni wananchi 42 ambao waliingia makubaliano hayo ya matumizi bora ya ardhi na makubaliao ya awali ilikuwa watafutiwe maeneo mengine ya makazi ili wapishe eneo hilo.