Mpanda FM

Zaidi ya bilioni 50 kutumika ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Katavi

20 July 2024, 10:34 pm

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe katika mkutano wa wadau wa kilimo cha umwagiliaji mkoa wa Katavi. Picha na John Benjamin

“Ujenzi Skimu ya uwagiliaji uliopo kata ya Mwamkulu halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi utagharimu kiasi cha fedha shilingi bilioni 31.6 na kutarajia kuhudumia zaidi ya wakulima 430.

Na John Benjamin -Katavi

Serikali nchini Tanzania imepanga kutumia zaidi ya bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya skimu ya uwagiliaji katika kata za Mwamkulu na Kabage mkoani Katavi.

Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe katika mkutano wa wadau wa kilimo cha umwagiliaji mkoa wa Katavi na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi skimu ya umwagiliaji uliopo kata ya Mwamkulu halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi itakayogharimu kiasi cha fedha shilingi bilioni 31.6 na kutarajia kuhudumia zaidi ya wakulima 430.

Sauti ya Waziri wa kilimo Hussein Bashe

Bashe amemwagiza Mkurungezi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji Tanzania Raymond Mndolwa kuhakikisha mwaka huu anatangaza tenda kwa wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa skimu za Kakese, Itenka na Karema ambapo amesema kuwa skimu hizo zilizopo wilaya ya Tanganyika na Mpanda zitakuwa na zaidi ya jumla hekari 50

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko katika mkutano huo amewataka Afisa Mtendaji na Afisa Kilimo mkoani Katavi kusimamia sheria na kanuni za kilimo cha umwagiliaji ili kuepukana na migogoro inayoweza kujitokeza

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko
Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph, wa pili kushoto Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko wakiwemo na viongozi wengine

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kilimo cha Umwagiliaji Tanzania Raymond Mndolwa amesema kuwa mkoa wa Katavi una jumla ya skimu 29 na kati ya hizo skimu 15 zimesajiliwa mpaka sasa ambapo ameeleza kuwa tume ya taifa ya umwagiliaji imeendelea kujipanga kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha mazingira ya wakulima.

Sauti ya mkurugenzi mkuu wa tume ya kilimo cha umwagiliaji taifa Raymond Mndolwa

Kwa upande wao wakulima kata ya Mwamkulu halmashauri ya ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamepongeza serikali kwa kuendelea kuwaboreshea miundo mbinu bora ya kilimo cha umwagiliaji na kuwaomba kuendelea kutoa elimu kupitia wataalamu wa kilimo ili waweze kufanya vizuri katika kilimo hicho cha umwagiliaji

Sauti za wakulima wakizungumza

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilianzishwa kwa Sheria ya Umwagiliaji Namba 4 ya mwaka 2013 ikiwa ni Idara inayojitegemea chini ya Wizara yenye dhamana ya umwagiliaji, tangu kuanzishwa kwake tume imefanya juhudi kubwa katika kuendeleza umwagiliaji nchini .