Rais Samia amaliza ziara mkoani Katavi, aridhishwa na maendeleo ya mkoa
16 July 2024, 10:21 am
“Ameridhishwa sana na maendeleo ya mkoa wa Katavi kwa kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia fedha za serikali zinazotolewa na serikali kuu kwa maendeleo ya mkoa.“
Na Samwel Mbugi -Katavi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake ya kikazi na chama katika halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe mkoa wa Katavi.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza eneo la Kibaoni amesema kuwa ameridhishwa sana na maendeleo ya mkoa wa Katavi kwa kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia fedha za serikali zinazotolewa na serikali kuu kwa maendeleo ya mkoa.
Pia amekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kusimamia na kufuatilia utendaji wa serikali kwa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa wakati.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amemshukuru Rais Samia kwa kusimamia na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami kwa mkoa wa Katavi.
Naye Waziri wa Maji Jumaa Hamidu Aweso amesema serikali inaendelea kutekeleza ilani ya chama kwa kuwawezesha wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe kwa kuhakikisha wanachimbiwa kisima cha maji kwa heshima ya Waziri Mkuu mstaafu Mizingo Kayanza Pinda.
Aidha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe Hamad Masauni ametangaza rasmi wilaya ya Mpimbwe kuwa makao makuu ya polisi ya wilaya kwa idhini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amehitimisha ziara yake ya kikazi na chama mkoani Katavi katika halmashauri ya Mpimbwe kwa kutoa shukrani kwa wananchi waliojitokeza katika mapokezi yake mpaka kuhitimisha ziara yake.