Mpanda FM

Rais Samia awataka viongozi jumuiya ya wazazi CCM kusimamia maadili

13 July 2024, 8:45 pm

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na wananchi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya wazazi yaliyofanyika mkoani Katavi. Picha na Samwel Mbugi

“Katika usimamizi wa maadili ya Mtanzania, jamii ya watanzania pia itakuwa karibu nao, pamoja na kushirikiana na taasisi kadhaa zisizo za kiserikali”

Na Samwel Mbugi-Katavi

Mwenyekiti  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM kuendelea kusimamia maadili ya vijana wa Tanzania ili kulifanya taifa kuendelea kuwa na nguvu kazi.

Rais Samia amebainisha hayo Julai 13, 2024 wilayani Mpanda mkoani Katavi wakati akifunga kilele cha Wiki ya Wazazi Kitaifa katika uwanja wa Azimio, ikiwa ni siku yake ya pili tangu alipowasili mkoani hapa kwa ajili ya ziara ya kikazi.

Amesema kuwa endapo jumuiya hiyo itakuwa karibu na jamii katika usimamizi wa maadili ya mtanzania, jamii ya watanzania pia itakuwa karibu nao, pamoja na kushirikiana na taasisi kadhaa zisizo za kiserikali ambazo zinazoshugulika na dawa za kulevya, ili kunusuru jamii kwenye janga la dawa za kulevya.

Sauti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika kiele cha maadhimisho hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Fadhili Maganya, amesema kuwa tatizo la malezi na maadili ni kubwa nchini na jitihada zinahitajika katika kuokoa kizazi cha sasa hivyo jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwaka 1955 imejipanga kuanzisha makongamano mbalimbali ili kulifikisha jambo hilo kwa jamii kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi.