Wazazi Katavi waaswa kutowaozesha mabinti katika umri mdogo
15 June 2024, 11:15 am
“Wazazi wanachangia mimba za utotoni kwa watoto wao kutokana na kuruhusu watoto hao kuwa na mahusiano katika umri mdogo“
Na Lilian Vicent -Katavi
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo hufanyika kila tarehe 16 Juni kila mwaka, halmashauri ya wilaya ya Nsimbo imefanya maadhimisho hayo katika kijiji cha Mtisi kitongoji cha Magula kata ya Sitalike ambapo wazazi wametakiwa kuacha kuwaozesha watoto wa kike wakiwa na umri mdogo badala yake wawaache wasome.
Hayo yamesemwa na diwani wa kata hiyo ya Sitalike Adam Chalamila wakati akiwahutubia wananchi hao na ameongeza kuwa mara nyingi wanapopokea kesi za wanafunzi waliopewa mimba zimekuwa zikiisha kwa makubaliano baina ya wazazi na watuhumiwa jambo ambalo halipaswi kufanyika hivyo .
Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii wa halmashauri hiyo Theresia Mwendapole amesema wameamua kufanya maadhimisho hayo eneo hilo kutokana na kuwa na changamoto za mimba za utotoni na ndoa za utotoni.
Nao baadhi ya wananchi wamesema ni kweli wazazi wamekuwa wakiwaozesha watoto wadogo na wengine wamekuwa wakiacha chuo na kutumikishwa kama wafanyakazi na wazazi wao.
Kauli mbiu katika maadhimisho ya Mtoto wa Afrika inasema ‘Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi’’