Watoto Wawili Familia Moja Wafariki kwa Ajali ya Moto
4 September 2023, 9:44 am
KATAVI.
Watoto wawili wa familia moja Florida Froline (3) na Ferisian Froline (3) wamefariki dunia Baada ya nyumba waliokuwemo kuungua Moto mtaa wa Tulieni kata ya Nsemulwa manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Shuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa watoto hao walikuwa ndani peke yao Wakati moshi mkubwa uliombatana na Moto kuonekana katika Nyumba hiyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Tulieni Hussein Kasomela amesema Baada ya Kupata taarifa amefika eneo la tukio kwa ajili ya kushirikiana na wananchi kuwaokoa watoto waliokuwa wahanga wa Mkasa huo.
Mkuu wa kitengo cha oparesheni kutoka jeshi la zima moto na uokoaji wilaya ya Mpanda Inspekta Geofrey Goerge Mwambungu amesema katika eneo la tukio pamekutwa na kiberiti ambacho kinadhaniwa kuachwa na mtu anaedhaniwa kufanya tukio hilo huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini katika uangalizi wa watoto.
Kwa upande wake kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa katavi ACP Kaster Ngonyani amefika eneo la tukio na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo.