Jamii FM

Wanafunzi wa chuo cha taifa cha ulinzi Tanzania (NDC) wafanya ziara mkoani Mtwara

14 January 2025, 09:20 am

Baadhi ya wanafunzi kutoka NDC wakipata maelezo ya awali juu ya hali kiuchumi na usalama kutoka kwa kanali Patrick Sawala Mkuu wa mkoa wa Mtwara (Picha na RS habari)

Hii ni ziara inayolenga kujifunza kwa vitendo waliyojifunza wakiwa darasani hasa katika miradi ya kiuchumi na usalama wa Wananchi kupitia miradi inayotekelezwa katika mkoa wa Mtwara.

Na Musa Mtepa

Mkoa wa Mtwara umepokea ugeni wa wanafunzi kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), waliofika mkoani hapa kwa lengo la kujionea hali ya kiuchumi, uzalishaji wa mazao, na usalama wa wananchi katika maeneo yao. Ugeni huu ni sehemu ya ziara ya mafunzo ya NDC, ambayo inalenga kuwapa wanafunzi fursa ya kuona maendeleo kwa Wananchi.

Akizungumza na vyombo vya habari January 13, 2025 kuhusu ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amesema dhamira kuu ya ziara hii ni kujionea hali ya usalama na maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wake.

Aidha amesisitiza kwamba mkoa wa Mtwara umejizatiti katika uzalishaji wa mazao na kuhakikisha usalama wa wananchi wake.

Sauti ya Kanali Patrick Sawala mkuu wa mkoa wa Mtwara
Baadhi ya wanafunzi kutoka NDC wakipata maelezo ya awali juu ya hali kiuchumi na usalama kutoka kwa kanali Patrick Sawala Mkuu wa mkoa wa Mtwara(Picha na RS habari)

Kwa upande mwingine, Brigedia Jenerali Erick Muhoro, Mkufunzi Mwelekezi Mwandamizi wa Mambo ya Anga kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), ameelezea kuwa ziara hii ni sehemu ya mafunzo ya wiki moja ambapo wanafunzi wa chuo hicho wanapata nafasi ya kujifunza na kutembelea maeneo yenye mafanikio ya kiuchumi na vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Mtwara.

Sauti ya Brig Jenerali Erick Muhoro mkufunzi NDC

Naye, Kanali Saidi Issa Abdala, mshiriki wa kozi ya Ulinzi wa Taifa kutoka NDC, amesema ziara hii ni sehemu ya utaratibu wa chuo cha NDC wa kulinganisha masomo ya darasani na hali halisi katika jamii. Ameongeza kuwa Mtwara ni miongoni mwa mikoa muhimu ambayo wanafunzi hao wanapaswa kutembelea kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo.

Sauti ya Kanali Saidi Issa Abdala mshiriki wa kozi ya ulinzi NDC

Ziara hiyo inatarajiwa kuendelea kwa wiki moja na itawawezesha wanafunzi hawa kupata maarifa muhimu kuhusu usalama, uzalishaji, na maendeleo ya kiuchumi mkoani Mtwara.