Kipindi: Wazee wa Kijiji cha Nanyati Mkoani Mtwara Wahimiza Uwekezaji Katika Elimu kwa Watoto
16 November 2024, 14:51 pm
“Korosho ni baraka kubwa kwa mikoa ya kusini, lakini tunapaswa kuangalia tunavyotumia mapato haya. Elimu ni uwekezaji wa kudumu kwa watoto wetu na jamii kwa ujumla, tofauti na sherehe ambazo hazina tija ya muda mrefu”
Na Msafiri Kipila
Wazee wa kijiji cha Nanyati, mkoani Mtwara, wamewataka wazazi kutoka mikoa ya kusini kuzingatia umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya watoto wao badala ya kutumia fedha nyingi kwenye sherehe za unyago, hasa wakati huu wa mavuno ya korosho.
Akizungumza, Yusufu Mmola mmoja wa wazee wa kijiji hicho, amesema kuwa licha ya wakulima wa mikoa ya kusini kufaidika na zao la korosho linaloingiza mapato makubwa, bado kuna tabia isiyofaa ya baadhi ya wazazi kutumia gharama kubwa zaidi katika sherehe za unyago kuliko katika masuala ya elimu.
“Korosho ni baraka kubwa kwa mikoa ya kusini, lakini tunapaswa kuangalia tunavyotumia mapato haya. Elimu ni uwekezaji wa kudumu kwa watoto wetu na jamii kwa ujumla, tofauti na sherehe ambazo hazina tija ya muda mrefu,” alisema Mmola.
Wazee hao wamewataka wazazi kubadilisha mtazamo na kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika kuboresha maisha ya watoto kwa kuwekeza katika elimu yao, jambo ambalo linaweza kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa vizazi vijavyo.