Takukuru Mtwara yaokoa zaidi ya shilingi milioni 31 za viuatilifu
11 November 2024, 15:52 pm
Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2024 TAKUKURU Mkoa wa Mtwara imepokea malalamiko 47 ambapo yanayohusu rushwa 37 na yasiyo husu rushwa yalikuwa 10.
Na Musa Mtepa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mtwara imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 31 za fedha za viuatilifu katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025.
Taarifa hii imetolewa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Jumbe Makoba, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo, Novemba 11, 2024, mkoani Mtwara.
Makoba ameeleza kuwa tukio hilo limetokea katika kijiji cha Chinyanyira, kata ya Sengenya, wilayani Nanyumbu ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2024, taasisi hiyo kupitia program ya TAKUKURU Rafiki ilikabiliana na changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Naibu Mkuu huyo, katika ufuatiliaji wa tukio hilo, jumla ya mifuko 604 yenye thamani ya fedha zaidi ya shilingi milioni 31, ilirejeshwa kwa wahusika na kuingizwa kwenye mfumo wa kugawiwa tena kwa wakulima waliokuwa wamekosa.
Makoba ameongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea na juhudi za kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na taasisi za umma, asasi za kiraia, viongozi wa dini, waandishi wa habari, na wananchi kwa ujumla, ili kutoa elimu kuhusu namna ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, na uchaguzi mkuu wa 2025.
Hii ni hatua nyingine ya TAKUKURU katika kudhibiti rushwa na kuhakikisha haki inatendeka katika sekta mbalimbali, hasa katika masuala ya kilimo na uchaguzi.