NERIO Mtwara yamwokoa mtoto akitumikishwa kazi ndani Dsm
30 August 2024, 18:13 pm
“Nashukuru kwa kunikomboa kwani nilikuwa nakutana na changamoto nyingi, nilikuwa nanyimwa chakula, mume wa bosi wangu alikuwa ananisumbua ananitaka kimapenzi kufika hapa salama nashukuru na hapa naungana na mama yangu na sitamuacha tena.“
Na Musa Mtepa
Kituo cha Msaada na Usaidizi wa Kisheria (NERIO) Paralegal Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara kimefanikisha kumrudisha binti mwenye umri wa miaka 14 aliyekuwa akitumikishwa kazi za ndani jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia tukio hilo Agosti 29, 2024 afisa tathmini na ufuatilia kutoka NERIO Paralegal Judith Chitanda amesema, mnamo Agosti 27, 2024 walipokea shauri kutoka kwa Bi. Kauri Momadi mama mzazi wa mtoto huyo raia na mkazi wa nchi jirani ya Msumbiji akiomba kusaidiwa kuonana na mtoto wake baada ya jitihada za awali alizofanya kugonga mwamba kutoka kwa mwajiri wa binti huyo kwa kudai kuwa kitendo hicho ni kinyume na matakwa ya mkataba waliokubaliana kati ya baba, dalali, mtoto na bosi wa kutoondoka au kusafiri katika eneo hilo ndani ya miezi sita .
Kwa upande wake Bi Kauri Momadi mama mzazi wa binti huyo ameelezea jinsi alivyopotezana na watoto hao huku akikishukuru kituo cha msaada na usaidizi wa kisheria kwa kumwezesha kuonana na mtoto wake.
Akizungumzia hali ya maisha aliyokutana nayo katika ufanyaji wake wa kazi za ndani, binti huyo amesema amekutana na changamoto nyingi ikiwepo ya kupigwa pamoja na kutakwa kimapenzi na mume wa mwajiri wake.
Musa Issa (19) mtoto wa kwanza wa Bi Kauri Momadi amesema alipokea simu kutoka kwa mama yake akiwa jijini Dar es Salaam alipokuwa akijitafutia maisha baada ya kuona maisha magumu aliyokuwa anayapitia akiwa kwa baba yake.
Aidha Mzee Issa Mohamedi Namiyuya baba mzazi wa binti uyo amesema kupitia tukio hilo amejifunza juu ya suala la ukatili na ajira kwa watoto kuwa siyo kitu kizuri huku akishangazwa na taarifa ya kuwa mtoto wake amewahi kukutana na changamoto ya kutakiwa kimapenzi na mume wa bosi wake.