Jamii FM
Jamii FM
30/03/2026, 10:10

Na Musa Mtepa
Wananchi wa vijiji vya Namuhi na Mnyija wamejikuta katika wakati mgumu wa mawasiliano kufuatia kukatika kwa daraja linalounganisha vijiji hivyo, baada ya kufurika kwa maji yanayotoka Bwawa la Kitere kupitia Mto Mambi unaotenganisha maeneo hayo.
Wakizungumza na Jamii FM Radio Machi 28, 2026, wananchi hao wamesema kuwa uharibifu huo umetokana na maji mengi kufurika kutoka Bwawa la Kitere, hali ambayo imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii, ikiwemo kilimo, usafirishaji pamoja na elimu.
Aidha, wameeleza kuwa kutokana na ulazima wa kuvuka katika eneo hilo, wamelazimika kuweka miti juu ya mto huo ili iwe njia ya kupita, jambo linalohatarisha usalama wao.

Hata hivyo, wananchi hao wameiomba serikali kufika katika eneo hilo kujionea hali halisi na kutatua changamoto hiyo ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kujitokeza.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Namuhi, Mwenyekiti wa kitongoji katika eneo lilipo daraja lililokatika, Bi. Suluhisho Nammanga, amesema athari zinazotokana na hali hiyo ni pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Namuhi na Shule ya Sekondari Libobe kushindwa kuhudhuria masomo. Pia, baadhi ya wakulima wameshindwa kufika mashambani kwa kuwa mashamba yao yapo upande wa pili wa mto.
Aidha, Bi. Suluhisho ametoa wito kwa serikali kutembelea eneo hilo na kuona umuhimu wa kujenga daraja hilo kwa haraka ili huduma muhimu kwa wananchi ziweze kuendelea kama kawaida.
Pia ameishauri serikali kwamba daraja litakapojengwa liwe refu zaidi kuliko lilivyokuwa awali, na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa kazi ya mkandarasi inakidhi matakwa ya mkataba husika wakati wa ukaguzi na makabidhiano.