ADEA yaendelea mafunzo ya uchongaji kwa vitendo
29 November 2024, 07:44 am
Huu ni mwendelezo wa mafunzo kwa vitendo kutoka kwa Wasanii wa Uchongaji ambapo leo wamepata mafunzo ya namna na jinsi gani ya kutengeneza bidhaa bora
Na Musa Mtepa
Wasanii wa sanaa ya uchongaji mkoani Mtwara wameonesha furaha na matumaini makubwa kutokana na mafunzo kwa vitendo wanayoendelea kuyapata kupitia shirika la ADEA, kupitia mradi wa kukuza na kuimarisha sanaa.
Wasanii hawa wamesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuwa mafundi bora na kutengeneza bidhaa bora, ambazo kwa sasa zinakutana na changamoto ya soko.
Steven Mohamed Mwanga, msanii wa uchongaji, amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kukuza na kuzalisha bidhaa bora zitakazosaidia kuongeza kipato na kuboresha soko la sanaa. Pia, amewashauri vijana kujitokeza kwa wingi katika fursa kama hizi ili kukuza vipaji na kuondoa vijana vijiweni bila kazi za maana.
Wasanii wengine, Paulina Frank na Magreth Ng’itu, wanaoshughulika na upigaji msasa, wamesifu mafunzo hayo kwa kusema kuwa yatawasaidia kutengeneza bidhaa bora na kukuza uchumi wao. Wameishukuru UNESCO na Alwaleed Philanthropies kupitia ADEA kwa kuwezesha mradi huu muhimu.
Kwa upande wake, Thiago Mtanda, mwezeshaji wa mafunzo hayo, amesema kumekuwa na mwitikio mzuri kutoka kwa wasanii, na matarajio yake ni kuona wasanii hawa wakifanya kazi za kisanaa bora zitakazowezesha kupata soko la uhakika.
Mtanda pia ameongeza kuwa mafunzo haya yatawasaidia wasanii kujitambua zaidi katika kazi zao za kisanaa na kuwa na mtandao mzuri unaotambulika na ADEA, ambao utawaunganisha na wadau watakaohitaji kazi zao za uchongaji.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Kuimarisha Sanaa, Utamaduni na Ufundi Stadi kwa Vijana, inayofadhiliwa na UNESCO na Alwaleed Philanthropies kupitia ADEA. Takribani vijana 50 kutoka Mtwara wanatarajia kunufaika nayo katika fani mbalimbali za sanaa, ikiwemo uchoraji, uchongaji, ufundi seremala na ufundi chuma.