Tanzania, CRCEG watia saini mkataba ujenzi miundombinu uwanja wa ndege Mtwara
29 April 2024, 20:23 pm
Bilioni 73.51 ni gharama za mradi wa usanifu na ujenzi wa jengo la abiria, vituo vya zimamoto na hali ya hewa pamoja na mnara wa kuongezea ndege ambazo zinaungana na bilioni 57 zilizotumika katika ujenzi wa eneo la kukimbilia ndege.
Na Musa Mtepa
Waziri wa Uchukuzi Mh. Prof Makame Mbarawa leo 29/4/2024 ameshuhudia hafla ya utiaji saini mkataba wa usanifu na ujenzi wa jengo la abiria, vituo vya zimamoto na hali ya hewa pamoja na mnara wa kuongozea ndege katika kiwanja cha ndege cha Mtwara kati ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania(TAA) na kampuni ya ujenzi ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG).
Akizungumza na wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya ndege vya Mtwara Waziri Prof. Mbarawa amesema serikali inaendelea kutekeleza miradi ya sekta ya uchukuzi na kuhakikisha Mtwara kunakuwepo kiwanja cha ndege kinachotoa huduma kwa saa 24 ili kukidhi viwango vya kiuendeshaji.
Aidha Waziri Prof. Mbarawa amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuhakikisha inatenga fedha za kutosha kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu ya uchukuzi nchini ili kuhakikisha inawezesha na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAA Musa Ibrahim Mbura amesema kuwa serikali tayari imesha tenga fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 73.51 kwa ajili ya utekelezaji wa mradio huo chini ya mkandarasi wa kimataifa China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) kwa kipindi cha miezi 36.
Akitoa Salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Daktari Samia Suluhu Hassani kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Mtwara.
Pia Mkuu wa Mkoa ameishukuru Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kuijali Mtwara huku akitumia nafasi hiyo kuomba Bandari ya Mtwara kuunganishwa na miundombinu ya usafiri wa reli kuelekea nyanda za juu ili kurahisish uchukuzi na usafirshaji wa mazao ya kilimo, migodi na bidhaa za viwandani.
Naye Katibu wa Siasa na Uenezi akimwakilisha mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mtwara Bw. Juma Hassani Namkoveka amesema ujenzi wa maradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi CCM ya Mwaka 2020/2025.