Mtenga akabidhi bati, TV kwa vijiwe vya bodaboda Mtwara
28 December 2024, 20:13 pm
Hii ni katika kuona anawafikia vijana kwenye maeneo yao ya kazi na kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili katika maeneo yao
Na Musa Mtepa
Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Mh. Hassani Mtenga, amekabidhi bati na televisheni zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5 kwa baadhi ya vijiwe vya bodaboda vilivyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani, Disemba 27, 2024. Msaada huu utatumika kujenga mabanda ya kupumzikia kwa vijana wa bodaboda wakati wa shughuli zao.
Akizungumza baada ya kukabidhi bati katika kijiwe cha Railway, Mh. Mtenga ameeleza kuwa mazingira ya kazi ya vijana wa bodaboda ni magumu, hasa kutokuwepo na maeneo ya kupumzika wakati wa masika (mvua) na jua kali.
Amesema vijana hao mara nyingi wanapozidiwa na hali ya mvua, wanajikuta wakirudi nyumbani na hivyo kukosa abiria. Kutambua changamoto hii, ametoa msaada huu kama ishara ya kuthamini kazi kubwa wanayoifanya vijana hao katika kutafuta riziki.
Aidha, Mh. Mtenga ametumia fursa hiyo kuzungumzia mafanikio yake katika uongozi na kuhimiza vijana wa jimbo lake kuepuka kufanya makosa ya kuchagua viongozi wasiokuwa na nia njema na wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini na Mkoa kwa ujumla.
Diwani wa Kata ya Reli, Ginfred Mbunda, ametoa shukrani kwa Mh. Mtenga kwa msaada alioutoa kwa vijana wa bodaboda na amewataka kuhakikisha msaada huo unatumika kama ulivyokusudiwa, na pia pale itakapojitokeza changamoto, wawasiliane na Mh. Diwani huyo ili kuona namna ya kukabilaiana nayo.
Mwenyekiti wa Kituo cha Bodaboda cha Reli, Charles Mponda, alitoa shukrani kwa msaada wa bati kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupumzikia, huku akimuomba Mh. Mtenga kuendelea kuwasaidia wananchi pale itakapojitokeza changamoto zinazoweza kutatuliwa na ofisi yake.
Hatua hii ya Mh. Mtenga inaonyesha juhudi za kutatua changamoto za vijana wa bodaboda na kuhakikisha kuwa wanakuwa na mazingira bora ya kufanya kazi.