Door of Hope Tanzania kutoa huduma ya msaada wa kisheria
28 June 2024, 18:18 pm
Huduma za msaada wa kisheria katika kituo cha msaada wa kisheria cha Door of Hope zitatolewa bure kwa kupitia vigezo kama vya kupitia mawakili waliopo kituonina kupitia kikosi kazi cha jumla ya watu 11
Na Musa Mtepa
Taasisi inayofanyakazi ya utetezi, uwezeshaji na usaidizi wa wanawake na vijana pamoja na kukuza masuala ya upatikanaji wa haki Door of Hope Tanzania leo Juni 28, 2024 imezindua rasmi huduma za msaada wa kisheria katika kituo cha msaada wa kisheria kilichopo mtaa wa Kiyangu Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Akizungmuza na waandishi wa habari kituoni hapo Mkurugenzi Mtendaji wa Door of Hope Tanzania Clemence Mwombeki amesema kuwa taasisi imekuwa ikitekeleza program na afua mbalimbali zinazolenga kulinda, kutetea na kukuza haki za binadamu hususani za makundi ya pembezoni ikiwepo Wazee,vijana ,Watoto ,wanawake na watu wenye ulemavu.
Aidha Mwombeki amesema kuwa Pamoja na uwezeshaji unaofanywa kwa makundi mbalimbali taasisi imebaini kuwa asilimia kubwa ya watanzania hawana uelewa wa haki zao za kiuchumi,kijamii,kisiasa na kitamaduni hivyo kupelekea wengi wao kutofahamu haki na wajibu hali inayopelekea wanapopatia huduma kwa viongozi wao kudhani wamepewa hisani.
Pia Clemence Mwombeki amesema kwa sasa kituo cha utoaji wa msaada wa kisheria kitajikita kwenye maeneo makuu saba ambayo mara kwa mara kituo kimekuwa kikipokea kesi kutoka kwa walengwa kama vile kesi zinazo husu haki za wanawake,Watoto ,Mirathi ,Ardhi, Masuala ya ndoa,Jinai na kesi zinazo husu madai.