Jamii FM

Wagombea wanawake Mtwara waelezea sababu za kugombea nafasi za uongozi

27 November 2024, 15:00 pm

Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa mtaa wa Ligula C Tatu Mbilinga akielezea sababu za kugombea nafasi hiyo

Huu ni uchaguzi wa serikali za mitaa wenye lengo la kuwapata viongozi wa mitaa,vijiji na vitongoji ambapo siku ya November 27, 2024, ndio utakuwa unafanyika ambapo kwa kipindi cha kunazia November 20 hadi 26,2024 kilikuwa kipindi cha kampeni kwa wagombea

Na Musa Mtepa

Baadhi ya wanawake wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa vijiji na mitaa kutoka vijiji vya Nyenged, Mnaida, na Mtaa wa Ligula C (Cocobeach) wilaya ya Mtwara, wameelezea sababu zilizowasukuma kugombea nafasi hizo.

Wakizungumza na Jamii FM Redio, tarehe 25 Novemba 2024, wanawake hao wamesema wanakusudia kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo yao, ikiwa ni pamoja na masuala ya maji, elimu, afya, na ukatili wa kijinsia.

Lukia Mnyachi, mgombea uenyekiti wa Kijiji cha Nyengedi, Kata ya Mkunwa, Halmashauri ya Mtwara Vijijini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema changamoto kubwa inayowakumba wanawake katika kijiji hicho ni upatikanaji wa maji.

Sauti ya Lukia Mnyachi, mgombea uenyekiti Kijiji cha Nyengedi.

Naye Tatu Mbilinga, mgombea uenyekiti wa Mtaa wa Ligula C (Cocobeach) kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema changamoto za barabara na maji katika mtaa huo ndizo zilizomvutia kugombea nafasi hiyo, huku akiahidi kuondoa kero hizo ikiwa atachaguliwa.

Sauti ya Tatu Mbilinga, mgombea uenyekiti Mtaa wa Ligula C.

Hawa Mohamedi Mniyanda, mgombea uenyekiti wa Kitongoji cha Mkunguni, kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Kijiji cha Mnaida, Kata ya Tangazo, Mtwara Vijijini, amesema ameguswa na umbali wa watoto kufuata elimu ya shule ya msingi, na kwamba akichaguliwa atahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake kutatua changamoto hiyo.

Sauti ya Hawa Mohamedi Mniyanda, mgombea uenyekiti Kitongoji cha Mkunguni.

Wagombea hawa wametoa wito kwa wananchi kutofanya kosa kwa kutowachagua, kwani wamedhamiria kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo yao.

Sauti ya wagombea wote wakielezea sera zao.