Rais Samia achangia milioni 100 ujenzi wa msikiti Tandahimba
27 November 2024, 11:54 am
Mskiti huu ukikamilika unakadiriwa kugharimi Shilingi milioni 450 ,ambapo vyanzo vikuu vya mapato vinavyotegemewa katika ujenzi wake ni michango ya waumini na wadau mbalimbali wanaojitokeza kuchangia kama alivyofanya Muheshimiwa Rais.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa mchango wa shilingi milioni 100 kwa waumini wa dini ya Kiislamu kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa msikiti wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mfano wa hundi ya mchango huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amesema kuwa nyumba za ibada ni muhimu katika jamii kwa sababu zina mchango mkubwa katika kulea kiimani na kimaadili mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
Kanali Sawala ametumia fursa hiyo kuwataka wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada za waumini wa Msikiti Masjidi Radhwa ili mradi wa ujenzi wa msikiti huo uweze kukamilika na kuanza kutumika.
Aidha, Kanali Sawala amewasisitiza viongozi wa msikiti kutumia mchango huo kwa uangalifu, kuendelea kuwa waadilifu, na kuhakikisha matumizi yake yanafanyika kwa uwazi ili kila mmoja aelewe hatua zinazochukuliwa katika mchakato wa ujenzi.
Akisoma taarifa kuhusu ujenzi wa msikiti huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Kasim Lihumbo, amesema kuwa gharama za jumla za ujenzi wa msikiti huo zinakadiriwa kuwa shilingi milioni 450, huku nguvu kubwa zikitakiwa kutoka kwa waumini na wadau mbalimbali ili kukamilisha mradi huo.
Kwa upande wake, Kaimu Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Shekhe Jamaldin Salimu Chamwi, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa mchango wake, na kuwasihi viongozi wanaosimamia ujenzi wa msikiti huo kuwa na mshikano na uadilifu ili mradi ukamilike kwa mafanikio.
Baadhi ya waumini walioshiriki katika hafla hiyo wameonesha furaha kutokana na mchango wa Rais,huku wakiomba wadau wengine kujitokeza ili kusaidia kukamilisha ujenzi wa msikiti huo kwa wakati.