Jamii FM

Polisi Mtwara wachunguza tukio la mtoto kujaribu kuua

27 January 2026, 18:11 pm

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara ACP Issa Suleiman akitoa taarifa ya matukio mbalimbali ya kihalifu kwa waandishi wa habari yaliyotokea mkoani Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linachunguza tukio la mtoto wa miaka 12 anayedaiwa kujaribu kumuua mtoto wa miaka 4 wilayani Nanyumbu. Wakati huo huo, polisi wamefanikiwa kukamata watuhumiwa wa nyara za serikali na dawa za kulevya katika oparesheni mbalimbali mkoani humo.

Na Musa Mtepa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linaendelea kuchunguza tukio la mauaji lililohusisha mtoto, lililotokea katika kijiji cha Masyalele, wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Januari 27, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Issa Suleiman, amesema mtoto Shabani Muebo (12) anadaiwa kujaribu kumuua mtoto mwenzake Ibrahimu Salumu Kelvine (4), wote wakazi wa kijiji cha Masyalele.

ACP Suleiman amesema tukio hilo lilitokea tarehe 23 Januari, 2026, ambapo mtuhumiwa alimlaghai mhanga aliyekuwa akicheza na watoto wenzake, kisha akaelekea naye katika msitu wa jando wa kijiji hicho na kumjeruhi shingoni kwa kutumia kiwembe kabla ya kumtelekeza katika pori.

Kamanda huyo ameongeza kuwa, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina wa tukio hilo, huku mtoto aliyedhurika akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Ndanda, wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Sauti ya 1 – ACP Issa Suleiman, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara

Katika hatua nyingine, ACP Suleiman amesema kupitia doria na misako inayoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa Wanyamapori, watuhumiwa wawili wamekamatwa kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali aina ya meno ya tembo.

Watuhumiwa hao ni Ignas Aron Mponzi (37), mwalimu wa Shule ya Msingi Namitende, na Dickson Ado (46), mkulima, wote wakazi wa kijiji cha Nangumbu wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

 Sauti ya 3 – ACP Issa Suleiman, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara

Vilevile, katika mwendelezo wa oparesheni za kupambana na uhalifu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara tarehe 17 Januari, 2026, liliwakamata Abas Mohamed Nakiti (49) na Mohamedi Mohamed Nakiti (22), wakulima na wakazi wa kijiji cha Mkachima wilayani Masasi, wakiwa na viroba kumi (10) vya dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa jumla wa kilogramu 110.

Sauti ya 4 – ACP Issa Suleiman, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limeeleza kuwa linaendelea kufuatilia na kudhibiti mbinu mbalimbali zinazotumiwa kufanya uhalifu, ikiwemo kupambana na usafirishaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya, ambavyo ni kinyume na sheria za nchi.