Jamii FM

Hospitali ya kanda yaibua furaha Mtwara

26 October 2025, 09:28 am

Mwonekano wa mbele wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Kusini iliyojengwa kata ya Mitengo Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa Mtwara wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, hatua iliyowapunguzia gharama na safari za kwenda Dar es Salaam kutafuta huduma za kibingwa, huku wakiiomba serikali kuendelea kuboresha huduma hizo kwa manufaa ya wananchi wa kusini

Na Musa Mtepa

Wananchi mkoani Mtwara wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuboresha huduma za afya kupitia Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyojengwa katika Kata ya Mitengo, Manispaa ya Mtwara-Mikindani.

Wakizungumza Oktoba 25, 2025, wananchi hao wamesema kuwa kabla ya kujengwa kwa hospitali hiyo, walilazimika kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam kufuata huduma za kibingwa. Wameeleza kuwa kwa sasa wanapata huduma hizo karibu, jambo lililopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu na usafiri.

Aidha, wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, hatua inayowanufaisha wakazi wa mikoa ya kusini pamoja na wananchi wa nchi jirani kupata huduma bora katika hospitali hiyo.

Sauti ya Wananchi wa Mtwara

Bi Hawa Mpai na Bi Hajrati Kuluthumu Mtonya, ambao ni miongoni mwa wagonjwa wanaopata matibabu katika hospitali hiyo, wameeleza kuridhishwa kwao na huduma zinazotolewa huku wakiiomba serikali kuendelea kuimarisha huduma za kibingwa ili kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Sauti ya Bi Hawa Mpai na Bi Hajrati Kuluthumu

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Benedect Ngaiza, amesema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini ina madaktari bingwa na madaktari bingwa wabobezi pamoja na vifaa tiba vya kisasa, ikiwemo vifaa vinavyopatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema kuwa upatikanaji wa huduma hizo umewezesha wananchi wa mikoa ya kusini kupata matibabu bora bila kulazimika kusafiri hadi Dar es Salaam.

Sauti ya Dkt. Benedect Ngaiza – Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
Chumba cha Dialysis kilichopo katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini (Picha na Musa Mtepa)