Jamii FM
Jamii FM
26 May 2025, 15:22 pm

Zahanati ya Mtawanya imekuwa ikihudumia Wananchi kutoka kata ya Mtawanya pamoja na vijiji Jirani kutoka halmashauri ya Mtwara vijijini hivyo uwepo wa jengo la nje wa wagonjwa(OPD) litasaidia kuondoa adha kwa wananchi hao.
Na Musa Mtepa
Mei 25, 2025 – Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwa zaidi ya kilomita 40 katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo umetembelea miradi sita ya maendeleo, ukiwemo ujenzi wa Zahanati ya Mtawanya, ambao umepewa pongezi kubwa kwa mchango wake wa kutatua changamoto za kiafya katika jamii.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD), Kiongozi Mkuu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ali Ussi, amesema mradi huo ni wa kimkakati na utaongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa kata ya Mtawanya.
Aidha, amewataka wananchi kuachana na tabia ya kuwatafutia changamoto madaktari wanaopelekwa kwenye vituo vya afya, akisisitiza kuwa ushirikiano kutoka kwa jamii ni nyenzo muhimu ya mafanikio.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mh. Shadida Ndile, amesema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo ni matokeo ya utekelezaji wa maagizo ya serikali kwa vitendo, kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akitoa taarifa ya mradi, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mtawanya, Dkt. Moses Chayeka, amesema kuwa kituo hicho kwa sasa kinahudumia wananchi zaidi ya 7,183 kutoka ndani na nje ya Manispaa hivyo ujenzi wa jengo jipya la OPD utapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano na umbali wa kufuata huduma, hususan huduma ya mama na mtoto.
Jengo hilo la OPD limejengwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 143.459, fedha zilizotolewa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya kuboresha huduma za afya katika ngazi ya jamii.