Jamii FM
Jamii FM
26 May 2025, 14:36 pm

Ni zaidi ya kilomita 40 mwenge umekimbizwa katika halmashauri ya Mtwara Mikindani huku ikipita katika miradi sita ya maendeleo ambapo yote mkimbiza Mwenge wa uhuru kitafa ameridhia utekelezaji wake
Na Musa Mtepa
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ndugu Ismail Ali Ussi, Mei 25, 2025, ametembelea na kukipongeza Kikundi cha Vijana cha Wajenzi Entrepreneur kilichopo Mbae Mashariki, Manispaa ya Mtwara Mikindani, ambacho kinajishughulisha na uzalishaji na uuzaji wa malighafi za ujenzi.
Katika hotuba yake, Ndugu Ussi ameeleza kuridhishwa kwake na jinsi kikundi hicho kilivyotumia vyema mkopo wa asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kupitia mapato ya ndani, kiasi cha Shilingi Milioni 32.7.

Aidha, ameipongeza Halmashauri hiyo pamoja na kikundi hicho kwa hatua yao ya kusajiliwa katika mfumo wa kidigitali wa NeST, hatua ambayo itawawezesha kushiriki kikamilifu kwenye zabuni na tenda zinazotolewa na serikali, akibainisha kuwa mfumo huo unathamini usalama na unamilikiwa na serikali tofauti na mfumo wa awali.
Kwa niaba ya Mwenyekiti wa kikundi, Ramadhani Ismail Mmogo amewasilisha taarifa ya mradi, akieleza kuwa ulianzishwa tarehe 1 Julai 2023 ukiwa na wanachama sita (wanaume wanne na wanawake wawili), na ulilenga kuwainua kiuchumi vijana kupitia biashara ya malighafi za ujenzi. Mradi huo umegharimu jumla ya Shilingi Milioni 39.7.

Ameongeza kuwa mikakati ya kikundi ni pamoja na kuwa taasisi kubwa inayotoa bidhaa bora za ujenzi kutoa ajira kwa wanawake na vijana,kupata eneo la kudumu kwa ajili ya ofisi ya kikundi.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 katika Manispaa ya Mtwara Mikindani zimepitia miradi sita ya maendeleo, ambayo ni kikundi cha Vijana Mbae Mashariki,Jengo la OPD Mtawanya,Shule ya Sekondari Tandika,ofisi ya Mtaa wa Majengo.mradi wa Maji – Mtaa wa Mwera, na kituo cha Redio cha HFM.