Jamii FM
Jamii FM
26/02/2026, 13:58

Mkurugenzi wa AGCOT na wizara ya kilimo wametaka wadau kukuza zao la embe, kuongeza tija, kuuza nje, na kuwapatia wakulima zana za kisasa ili kuongeza mapato na maendeleo ya kilimo
Na Musa Mtepa
Mkurugenzi Mkuu wa AGCOT, Geoffrey Kirenga, amewahimiza wadau wa kilimo kuendeleza na kuinua zao la embe katika soko la ndani na la kimataifa ili kuongeza kipato cha wakulima na kupunguza utegemezi wa zao la korosho pekee.
Akizungumza Februari 18, 2026, baada ya Warsha ya Wadau wa Kilimo iliyolenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uendelezaji na ukuzaji wa Shoroba za Kilimo kwa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara, iliyofanyika mjini Mtwara, Kirenga amesema kuna fursa kubwa katika uzalishaji wa embe kwa kuongeza thamani na kuuza nje ya nchi, hatua itakayoongeza mapato ya fedha za kigeni kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

Kirenga ameeleza kuwa endapo zao la embe nchini litaendelezwa ipasavyo, soko lake Duniani linaweza kufikia zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 75 kwa mwaka, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 187.5 za Tanzania, kiasi kinachokadiriwa kuwa takribani mara tatu ya mapato yanayotokana na zao la korosho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo katika Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Elizabeth Misokia, amesema shoroba za kilimo zimeanzishwa kwa lengo la kuweka mikakati madhubuti ya kukuza sekta ya kilimo kupitia ongezeko la uzalishaji, ajira na mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wakulima ili waweze kunufaika kibiashara.
Aidha, Misokia amesema licha ya mipango thabiti inayotekelezwa na Serikali, bado wakulima wengi wanatumia zana duni kama majembe ya mkono. Hivyo, Serikali imejipanga kuwapatia wakulima zana za kisasa zikiwemo matrekta, elimu ya kilimo bora pamoja na mbegu bora ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Akizungumzia changamoto ya kilimo kinachotegemea mvua, Misokia amesema Serikali inapanga kuboresha na kuongeza mabwawa ya maji, kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za maji, pamoja na kushirikiana na sekta binafsi ili kuwawezesha wakulima kuendesha kilimo cha kisasa chenye miundombinu rafiki kwa uzalishaji wa mwaka mzima.