Jamii FM
Jamii FM
26 January 2026, 10:12 am

Vijana wa Kata ya Chuno, Mtwara Mjini, wametakiwa kuungana katika vikundi ili kunufaika na tenda na mikopo ya serikali kwa maendeleo yao ya kiuchumi
Na Musa Mtepa
Vijana wametakiwa kuungana na kuunda vikundi vitakavyowawezesha kupata tenda na mikopo kutoka serikalini, hatua itakayosaidia kuinua uchumi wao binafsi na jamii kwa ujumla.
Wito huo umetolewa tarehe 25 Januari, 2026 na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Mtwara Mjini, Ndugu Nassoro Mohemedi, wakati wa Kongamano la Vijana lililofanyika katika Kata ya Chuno.
Akizungumza katika kongamano hilo, Ndugu Mohemedi amesema kuwa vijana wana uwezo wa kujijenga kiuchumi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja iwapo watajipanga vizuri na kutumia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri, sambamba na shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliohudhuria kongamano hilo wamesema wamejifunza mambo mbalimbali, ikiwemo kutambua fursa zilizopo katika maeneo yao. Aidha, wamewapongeza viongozi wa kata hiyo kwa kuwaandalia kongamano hilo lenye manufaa makubwa kwa maendeleo yao.

Naye mratibu wa kongamano hilo, Iddi wa Mangongo, kwa kushirikiana na Diwani wa Kata ya Chuno, amesema kuwa lengo kuu la kufanyika kwa kongamano hilo ni kutokana na kutambua kuwa vijana ni kundi kubwa na muhimu katika jamii, hivyo wanapaswa kuelimishwa na kupewa taarifa kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika maeneo yao.
