Jamii FM

Vikundi vya Jogging Mtwara vyahamasisha uchaguzi wa Amani

25 October 2025, 14:45 pm

Vikundi kumi vya Jogging vikishiriki katika mbio fupi zilizoanzia katika viwanja vya Mashujaa hadi hospitali ya Rufaa ya kanada ya Kusini iliyopo Mitengo Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)

Vikundi kumi vya jogging Mtwara Mikindani vimeshiriki mbio fupi kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, zikiwa na kaulimbiu “Mazoezi kwa Afya, Uchaguzi wa Amani ni Msingi wa Maendeleo.”

Na Musa Mtepa

MTWARA-Vikundi kumi vya jogging kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani leo Oktoba 25,2025 vimeshiriki katika mbio fupi zilizoandaliwa kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 kote nchini.

Mbio hizo zilizoanzia katika Viwanja vya Mashujaa, Manispaa ya Mtwara Mikindani na kumalizikia katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara.

Washiriki wa mbio hizo wamesema mazoezi ni muhimu kwa afya kwani husaidia kuzuia magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na matatizo ya afya ya akili.

Sauti ya washiriki wa mbio fupi

Aidha, Bi Fatuma Jana na Martin Deo wametumia nafasi hiyo kuhamasisha wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuchagua viongozi bora watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Washiriki hao pia wamesisitiza umuhimu wa kupiga kura kwa amani na utulivu kwa kufuata maelekezo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ikiwemo kurejea nyumbani baada ya kupiga kura na kusubiri matokeo kutangazwa rasmi.

Sauti ya washiriki wa mbio fupi

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Ndugu Abdala Mwaipaya, amesema anajivunia kuwa katika wilaya ambayo wananchi wake wanapenda kufanya mazoezi na kujali afya zao. Amesema hatua ya kumalizia mbio katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini ni ishara ya kuonesha uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya afya.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdala Mwaipaya
Mkuu wa wilaya ya Mtwara akizungumza na washiriki wa mbio fupi baada ya kufika katika Hospitali ya Rufaa kanda ya kusini iliyopo Mitengo Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Benedect Ngaiza, amesema kufanya mazoezi ni njia bora ya kuepuka magonjwa yasiyoambukiza na kuboresha afya kwa ujumla. Pia amewashauri wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya ya miili yao.

Sauti ya Dkt. Benedect Ngaiza, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara

Haya ni mazoezi yaliyohusisha vikundi kumi vya mazoezi(Jogging) vilivyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo kupitia mazoezi hayo yalibeba ujumbe wa “Mazoezi kwa Afya,Uchaguzi wa Amani ni Msingi wa maendeleo”Kupiga kura ni haki yako.