CCM yaitaka CBT koboresha mfumo wa usambazaji pembejeo kwa wakulima
25 July 2024, 07:51 am
Kitendo cha kuwepo kwa madalali kwenye zao la korosho ndiyo sababu mojawapo inayochangia wakulima kutonufaika na kile alichokilima pamoja na mfumo wa mnada unaofanyika sasa hivi wa kutokuwepo mhusika aliyeweka barua ya ununuzi wa korosho hizo.
Na Musa Mtepa
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mtwara Vijijini Nashiri Pontiya ameitaka Bodi ya Korosho Tanzania kuboresha mfumo wa usambazaji wa pembejeo za zao la korosho ili kuondokana na changamoto zinazowakabili wakulima vijijini.
Hayo ameyasema kwenye kikao cha ushauri wilaya Mtwara (DDC) kilichofanyika Julai 23, 2024 katika chuo cha ualimu Mtwara (TTC KAWAIDA) kilichojadili Dira ya taifa ya maendeleo ya Mwaka 2025/50 ambapo amesema kuwa changamoto zimekuwa nyingi juu ya mfumo wa usambazaji wa pembejeo kwa wakulima pamoja na kuwashirikisha viongozi wa serikali za mitaa katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya pembejeo zinazotolewa.
Wakichangia mapendekezo ya nini kifanyike kupitia dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025/50 wadau wa kilimo kupitia zao la korosho na Mwani wamependekeza kutokuwepo kwa madalali (mtu kati)kwenye minada ya zao la korosho ili kumsadia na kumnufaisha mkulima zao hilo.
Kwa upande wa mkurugenzi mtendaji wa bodi ya korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred amesema moja ya changamoto kubwa iliyopo kwa wakulima ni kutoridhika na kipato anachokipata kutoka kwenye mazao hivyo ili kuondoa changamoto hizo na katika kutekeleza dira ya taifa ya maendeleo wilaya na mkoa kwa ujumla kuangalia namana gani mkulima aweze kumiliki viwanda vya kubangulia korosho ili kuzipa thamani na kuachana na mtu kati wa zao la korosho.